Unapousikia au kuutazama wimbo
ulioimbwa na kwaya ya Kanisa la Memonite Tabata, “WANA KUNYATANYATA ”(Menonite
Tabata Choir) unaweza kujiuliza ni nani yule mwimbaji wa kiume anayeonekana
kiongozi na mwimbaji mkuu wa kwaya hiyo iliyovuma sana miaka ya 2000 mpaka
2010 nchini Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Wengi ukiwauliza
watakujibu pengine ni kiongozi tu wa kwaya hiyo, wengine hudhani labda ni
mwinjilisti au hata mchungaji katika kanisa hilo.
Si watu wengi wanaolifahamu jina
lake halisi wala historia yake kwa ujumla. Binafsi ni mpaka hivi karibuni
wakati nikisikiliza kipindi kimoja cha redio TI FM kijulikanacho kama
Gospel Vibration kinlichorushwa hewani siku ya Jumatano Alasiri ndipo nikabaini
kuwa mwimbaji huyo maarufu anajulikana kwa jina la ELIKANA SIMATYA MBIJIMA
mzaliwa wa Mkoa wa Dodoma.
Mwimbaji Elikana Simatya anasema
kuwa alianza kuimba alipokuwa na miaka 5 hapo mwaka 1975 baada ya kuwa alikuwa
akiiba gitaa la kaka zake walipotoka na kuanza kujifunza kupiga mwenyewe. Baada
ya kaka zake hao kubaini kuwa mdogo wao alikuwa na kipaji kikubwa cha uimbaji
na tayari alikuwa ameshaanza kujua kupiga gitaa ndipo sasa walipoamua rasmi
kumruhusu kulichezea gitaa hilo kwa nafasi kwa lengo la kujifunza zaidi.
Anasema katika maisha yake ya
uimbaji amewahi kuwa mwalimu wa kwaya mbalimbali jijini Dar es salaam ikiwemo
hii ya kanisa la Menonite Tabata ambayo alihudumu nayo mpaka mwaka 2008
alipoachana nayo na kujiunga na kwanya nyinginezo jijini Dar es salaam. Yeye
Kama Mwalimu huwa anaitwa na makanisa mbalimbali ambapo baada ya mazungumzo
huanza kuzifundisha kwaya za makanisa hayo. Alipoulizwa ni kwanini asianzishe
uimbaji binafsi kama wafanyavyo waimbaji wengi siku hizi alijibu kwamba, swali
hilo amewahi kuulizwa na watu wengi ambao mwisho wake humcheka na
kumwambia kwanini anakufa masikini wakati ana kipaji kikubwa namna ile, lakini
yeye huwajibu kuwa huduma anayoitoa si kwa ajili ya kupata faida
inayoonekana kwa macho ya nyama bali zaidi ni kwa ajili ya kuwagusa watu katika
kumwabudu Mungu.
Akitolea mfano wa albamu hiyo ya
kunyatanyata, anasema kuwa kipindi hicho iliingiza fedha kiasi kikubwa karibu
shilingi milioni 90 za Kitanzania lakini zilikuwa ni mali ya kwaya na kanisa na
wala siyo mali ya mtu mmojammoja.
Elikana Simatya pia alitaja
sababu kubwa inayochangia kudorora kwa kwaya nyingi siku hizi tofauti na kama
ilivyokuwa miaka michache iliyopita kuwa ni kukosekana kwa motisha kwa
wanakwaya mfano wanakwaya hupendelea kupata ziara kwenda kuimba makanisa
mengine au mialiko mbalimbali lakini hawapati fursa kama hizo jambo
linalowapunguzia motisha wa kuendelea kuimba.
Halikadhalika pia suala la
maslahi, wanakwaya wengine hawana ule moyo wa kuona mapato ya kwaya yakiendelea
kuwa mali ya kanisa kwa ujumla wakati wao wenyewe ndio wanaoimba, anasema kwa
mfano katika kanisa la Menonite Tabata nyakati hizo uongozi wa kanisa uliamua
kwaya kuwa na akaunti ili kusimamia mapato yao wenyewe na ilichangia sana
mafanikio ya kwaya hiyo. Anashauri makanisa kujali maslahi na motisha kwa
wanakwaya ili kurudisha msisimko wa kwaya uliokuwepo miaka ya nyuma badala ya
waimbaji wengi kukimbilia kuimba binafsi au katika nyimbo za kidunia.
Bwana Elikana ana mke mmoja na
watoto watatu ambao kati yao wawili tayari wamekwisha olewa huku mmoja bado
akiwa anaendelea na masomo yake.
Pamoja na Bwana Elikana Simatya
kwa sasa kuwa anaendelea na shughuli za kufundisha kwaya mbalimbali za makanisa
jijini lakini bado ana nia ya kutoa kazi zake binafsi na anasema tayari kuna
albamu yake nzima aliyoiandaa miaka 10 iliyopita lakini ikakwama studio
kutokana na mgogoro wa kimaslahi baina ya mzalishaji wa albamu hiyo na muuzaji.
Hata hivyo anasema bado anayo nia ya kuitoa kazi yake hiyo na anaamini kutokana
na uzuri wake ni lazima itafanya vizuri sokoni. Kazi zake mbalimbali alizozitoa
mwenyewe mbali na zile alizozitoa akiwa na kwaya mbalimbali zipo katika mtandao
wa You tube na link zake zimewekwa hapo chini.
Blogu hii ipo chini ya Bwana Elikana Simatya mwenyewe na makala na michango ya mawazo hutoka kwa mashabiki wake mbalimbali wa zamani na pia wa sasa hivi. Hata hivyo Nyimbo zote alizoimba na kwaya mbalimbali ikiwemo Tabata Mennonite ukiacha zle zilizoimba binafsi kama ule wa Msafiri zimewekwa hapa kwa hisani ya kwaya hizo na si kama mali binafsi ya Mwalimu Elikana Simatya.
0 Response to "Mwimbaji wimbo wa kunyatanyata Menonite Tabata Choir, Elikana Simatya"
Post a Comment